Ligi ya Uganda ni bora Zaidi Afrika Mashariki adai Joseph Owino
Beki wa zamani wa klabu ya Simba na Azam, Joseph Owino amezungumzia ubora wa ligi kuu za nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Owino ambaye ni nahodha wa zamani Simba amecheza kwenye ligi zote tatu na kudai ligi ya Uganda ni bora Zaidi kiushindani kuliko Tanzania na Kenya.
Akizungumza na mtandao wa Soka360, kuhusu kufuzu mfululizo kwa Uganda kwenye michuano ya CHAN huku Kenya ikiwa haijawahi kufuzu na Tanzania ikiambulia mara moja, Owino amehusisha moja kwa moja jambo hilo na ubora wa ligi ya Uganda.
“Ligi ya Uganda ina wachezaji bora zaidi na wachapakazi kulinganisha na wale wa Tanzania na Kenya, ndio maana Uganda haipati taabu kufuzu CHAN”
Kwa upande wa Tanzania na Kenya, Owino anaona ligi ya Kenya ina nafuu kidogo ya ushindani kuliko Tanzania licha ya kuzidiwa kwa udhamini na mvuto wa mashabiki na ligi ya Tanzania.
Baada ya kuachana na Simba mwishoni mwa msimu uliopita, Owino alijiunga na klabu ya Sofapaka ya Kenya ambayo nayo amevunja mkataba baada ya kutolipwa kwa miezi saba.
No comments