Recent Posts

JUMA NYOSO AZUNGUMZA KWA MARA YA KWANZA TANGU APEWE ADHABU NA TFF

Juma Said Nyosso, beki na nahodha wa kikosi cha Mbeya City amefungiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania  (TFF) kujihusisha na masuala
ya soka kwa miaka miwili na faini ya shilingi milioni mbili za kitanznia kwa kosa la kumdhalilisha John Bocco wa Azam FC
Baada ya TFF kumpiga kufuli mchezaji Juma Nyosso kujihusisha na masuala ya soka, mchezaji huyo ameibuka na kuzungumza kwa mara ya kwanza tangu aanze kutuhumiwa kumdhalilisha nahodha wa Azam FC John Bocco.
Nyosso amesema uongozi wa klabu yake ulimwambia asizungumze chochote kuhusu tukio hilo hadi pale atakapoitwa na TFF au uamuzi wa TFF utakapotoka. Mara baada ya TFF kutoa adhabu kwa mchezaji huyo, Shaffidauda aliamua kumtafuta Nyosso na kufanya nae mazunumzo kutaka kujua amechukuliaje adhabu aliyopewa na TFF.
Hapa chini utapata majibu yote ya maswali yako kwa Nyosso kuhusiana na tukio zima lilivyotokea na adhabu aliyopewa na TFF.
Shaffihdauda: Baada ya kupewa adhabu na TFF ya kufungiwa kucheza soka kwa miaka miwili pamoja na faini ya shilingi milioni mbili, wewe unazungumziaje adhabu hiyo ukilinganisha na kosa lenyewe?
Juma Nyosso: Mimi nadhani hao viongozi walionihukumu mimi, walifanya haraka sana bila kufanya utafiti wa umakini zaidi, mimi nadhani nimeonewa kwasababu ya utashi wa watu lakini wakifatilia ushahidi zaidi kwasababu video ipo, wangefatilia vizuri ili waje watoe hukumu sasa wameshatoa hukumu na video inajidhihirisha.
Naomba wafatilie ile mechi yote kuna mambo mengi yalikuwa yanatokea kwenye ile mechi mpaka wakafikia wao kuhisi labda mimi nimefanya kile kitendo. Mimi ni mtu mzima siwezi kurudia kitendo ambacho klabu yangu na TFF ilishanihukumu siwezi kufanya vile hata siku moja.
Ndio maana mimi nimekaa kimya muda mrefu kusikiliza itakuwaje na klabu ikaniambia nisiongee na mtu yoyote tusubiri tuone itakuwaje. Mwisho wa siku nikasikia nimefungiwa miaka miwili, unamfungia mtu miaka miwili bila ushahidi uliokamilika nadhani kama walikurupuka au walitumia jazba.
Shaffihdauda: Baada ya TFF kutangaza adhau ya kukufungia kwa miaka miwili na faini ya shilingi milioni mbili, wewe adhabu hii uliipokeaje?
Juma Nyosso: Nimeumia sana kwasababu mimi maisha yangu ni mpira halafu leo unaniambia umenifungia miaka miwili na faini milioni mbili halafu ni kitu ambacho mimi najua sikukifanya yani nimeumia sana ndio maana watu wengi walikuwa wananipigia lakini mimi nilikuwa sitaki kuongea.
Kwasababu viongozi wangu baada ya kufatilia ile video imeonekana kila kitu, ndio maana mimi nimeruhusiwa kuongea. Angalia Bocco alivyokuwa akinifanyia rafu za waziwazi lakini mwamuzi alikuwa hafanyi chochote, kwavile mimi najulikana Nyosso tambia zangu za huko nyuma wanachukulia kwa utashi wao wanakuja kunihukumu miaka miwili.
Shaffihdauda: Ukiangalia ile video inaonekana kulikuwa na majibizano kati yako na baadhi ya wachezaji wa Azam, kitu gani kilikuwa kinaendelea?
Juma Nyosso: Pale yalikuwa majibizano tu ya uwanjani kwamba, cheza mpira basi ikatokea hivyo. Mwisho wa siku naoneshwa picha lakini viongozi wakaniambia nikae kimya kwanza. Wamefatilia wakaniambia sasa naweza kuweka wazi.
Shaffihdauda: Adhabu imeshatoka sasa nini kinafata sasahivi kuanzia wewe mpaka timu yako ya Mbeya City kuhusiana na adhabu uliyopewa na TFF.
Juma Nyosso: Nadhani klabu yangu itafatilia hili suala kama ni kukata rufaa na kwavile kuna chama cha wachezaji SPUTANZA, watalivalia njuga hili suala ili kufatilia haki za mchezaji, haiwezekani unifungie miaka miwili wakati mpira ndio kazi yangu unategemea miaka miwili mimi nikae nyumbani tu.
Shaffihdauda: Kabla ya tukio ambalo limepelekea wewe kufungiwa, kulikuwa na matukio mengine ambayo wewe ulifanyiwa katika mchezo huo dhidi ya Azam?
Juma Nyosso: Matukio mengi sana ndio maana nasema video inajidhihirisha, wakae kama kamati ya nidhamu kama ndio bodi ya ligi waangalie video yote matukio niliyokuwa nafanyiwa mimi halafu watajiridhisha kwenye hiyo hukumu yao.

No comments