Recent Posts

Yanga, Azam zashindwa kutambiana (+ pichaz)


Kipre Tchetche (aliyekaa chini) akipongezwa na wachezaji wenzake baada ya kuifungia Azam goli la kusawazisha kwenye mchezo kati ya Azam FC dhidi ya Yanga

Timu za Yanga na Azam zimeshindwa kutambiana kwa mara nyingine tena baada ya kulazimishana sare ya kufungana goli 1-1 kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara uliochezwa leo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga ndio walikuwa wa kwanza kupata goli dakika ya 45 kipindi cha kwanza mfungaji akiwa ni mshambuliaji wao tegemezi Donald Ngoma ambaye alifunga goli hilo kwa ustadi mkubwa baada ya kupokea krosi kutoka kwa Juma Abdul na kuwatoka mabeki wa Azam kisha kupachika mpira wavuni.

Mshambuliaji wa Yanga Donald Ngoma akishangilia goli aliloifungia timu yake wakati ikicheza dhidi ya Yanga

Goli hilo liliwafanya Yanga kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa goli 1-0 dhidi ya Azam FC.

Kipindi cha pili Azam walirejea kwa kasi wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara huku wakimiliki mpira kwa dakika za katikati ya kipindi cha pili wakati Yanga kwa upande wao walikuwa wakicheza mipira mirefu na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Beki wa Yanga Haji Mwinyi akiruka kukwepa kwanja la Agrey Morris

Kipre Tchetche aliyeingia kipindi cha pili kuchua nafasi ya Alan Wanga aliifungia Azam goli la kusawazisha dakika ya 83 akiunganisha pasi ya Farid Musa na kuufanya mchezo kuwa sare kwa goli 1-1.

Wakati dakika zikiwa zimeyoyoma, Yanga walipata penati baada ya golikipa wa Azam Aishi Manula kumwangusha mchezaji wa Yanga Simon Msuva kwenye eneo la hatari lakini Manula alipangua penati hiyo iliyopigwa na Thabani Kamusoko.

Mashabiki wa Yangawakifurahia goli liliofungwa na Ngoma

Mwamuzi wa mchezo huo Abdallah Kambuzi kutoka Shinyanga aliingia kwenye mgogoro na baadhi ya wachezaji wa Azam FC ambao walikuwa wakipinga penati iliyoamriwa kupigwa kuelekezwa kwenye lango la Azam wakidai haikua halali.

Nahodha wa Azam FC John Bocco akiwatuliza wachezaji wenzake waliokuwa wakimzonga mwamuzi wa mchezo huo

Timu hizo zilitoka sare pia kwenye mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kagame Cup mwezi Julai mwaka huu na Azam wakasonga mbele kwa ushindi wa mikwaju ya penati.

Timu hizo zilikutana tena kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii mapema mwezi Septemba mwaka ambapo dakika 90 za mchezo huo zilimalizika kwa sare, Yanga alitwaa ubingwa huo kwa mikwaju ya penati

No comments