MAGUFULI CUP YAZINDULIWA RASMI, ABAJALO YAANZA KWA USHINDI
Timu ya Abajalo SC leo imeifungta
timu ya Zakhem SC kwa goli 2-1 kwenye mchezo wa ufunguzi wa michuano ya
Magufuli Cup ‘#Hapa Kazi Tu’ iliyoanza kutimua vumbi rasmi leo kwa
mchezo mmoja uliochezwa kwnye uwanja wa Mwl. Nyerere, Magomeni jijini
Dar es Salaam.
Magoli yote mawili ya Abajalo
yamefungwa na Lameck Daiton, goli la kwanza limefungwa dakika ya tisa
wakati goli la pili limefungwa dakika ya 11 kwa mkwaju wa penati baada
ya Muhsin Said kuangushwa kwenye eneo la hatari wakati akielekea kufunga
goli la pili.
Goli pekee la Zakhem limefungwa
na Muhsin Ngalanda kwa kichwa baada ya timu hiyo kutengeneza nafasi
nzuri na Ngalanda kuitumia vyema nafasi hiyo kuukwamisha mpira wavuni na
kuipa timu yake goli la kufutia machozi kwenye mchezo wao wa kwanza.
Mchezo huo wa ufunguzi ulikuwa ni
mkali na wakuvutia uliokutanisha wachezaji wenye uwezo na vipaji vya
hali ya juu ambapo umati mkubwa wa mashabiki walijitokeza kushuhudia
pambano hilo.
Idd Azan ambaye ni mgombea Ubunge
wa Jimbo la Kinondoni kwa tiketi cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiye
aliyezindua mashindano hayo akiongozwa na Madee ambaye ni msanii wa
kundi la muziki la Tip Top Connections ambao ndio wandaaji wa mashindano
hayo.
Azan amesema, mashindano hayo
licha ya kutoa nafasi kwa vijana kuonesha vipaji vyao, lakini michuano
hiyo ina lengo la kuwakumbusha wachezaji na wapenzi wote wa soka kupiga
kura kwa amani kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 25
mwaka huu.
Mgombea huyo pia amelipongeza
kundi la Tip Top Connections kwa kuandaa mashindano hayo hasa kwa
kipindi hiki cha kampeni ili kuwaweka watu tofauti pamoja na
kuwakumbusha kuhusu umuhimu wa kuchagua viongozi bora watakao watumikia
kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Naye Madee kwa niaba ya Tip Top
Connections amemshukuru Bw. Azan kwa kukubali kufungua mashindano ya
Magufuli Cup na kuzungumza na vijana kuhusu masuala mbalimbali
yanayohusu uchaguzi mkuu.
Michuano hiyo itaendelea tena
Jumamosi (kesho) kwa timu za Tuamoyo na Burudani kuoneshana kazi kwenye
uwanja wa Machava, Kigamboni.
No comments