Recent Posts

Jinsi Taifa stars itakavyoitoa Algeria


Taifa Stars inatarajiwa kuikabili Algeria tarehe 9 Novemba 2015 Tanzania wakiwa nyumbani na 17 Novemba ugenini Algeria

Japo bado safari ni ndefu na si mara ya kwanza kwa makocha wa Taifa Stars kuanza kwa kutupa matumaini, si dhambi tukimvika joho la ufalme japo kwa muda, kocha Mkwasa kwa angalau kuifanya Taifa Stars kutoka kwenye kundi la kero za Mtanzania.

Kwa matokeo ya kuridhisha dhidi ya Uganda, Nigeria na hatimaye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Malawi licha ya kufungwa 1-0 ugenini Malawi, kasia la mzawa Mkwasa linaonekana kupita kwenye bahari iliyokuwa ngumu kupitika kwa boti ya injini ya mzungu Marti Maria Ignatius Nooij.

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inahitaji kufanya mabadiliko makubwa kufuatia kipigo cha 1-0 dhidi ya Malawi katika hatua za awali mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2018 huku wakiwa na tumaini kuwa kocha mpya ataleta mwanga wa mafanikio.

Stars imefanikiwa kufuzu hatua ya kwanza ya mchujo baada ya kuifunga Malawi 2-0 Dar es salaam, ushindi pekee dhidi ya The Flames ambao unaipa Tanzania fursa ya kuikabili Algeria katika hatua inayofuata baada ya kupoteza mechi ya marudiano mjini Blantyre.

Taifa Stars inatarajiwa kuikabili Algeria tarehe 9 Novemba 2015 Tanzania wakiwa nyumbani na 17 Novemba ugenini Algeria.

Hebu tuone. Je! Tanzania ina kikosi thabiti chenye uwezo wa kuikabili Algeria na kuifunga? Mara ya mwisho Stars kukutana na Algeria matokeo yalikuwaje? Nini kifanyike ili Stars wawe na uwezo mzuri kuwakabili Mbweha wa Kijani “El Khadra”.

Ufuatao ni uchambuzi wa Algeria katika michuano mbali mbali ya hivi karibuni, mfumo wa uchezaji wao, Kombe la Dunia na aina ya wachezaji walio nao.

Historia yao katika fainali FIFA za Kombe la Dunia

Algeria wameshiriki michuano ya Kombe fainali za Kombe la Dunia za FIFA mara nne, ikiwa pamoja na ile ya Brazili 2014 ambako walifika hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza – hatua kubwa zaidi tangu waanze kushiriki. Katika michuano minne wameshinda jumla ya mechi tatu, ambazo walishinda kule Hispania 1982 dhidi ya Ujerumani (2-1) na Chile (3-2). Al Khadra walipata ushindi wa tatu kule Brazili, walipoifunga Jamuhuri ya Korea 4-2, na kuwa nchi ya kwanza Afrika au ya Kiarabu kufunga magoli manne michuano ya Kombe la Dunia katika mechi moja.

Kikosi chao

Baada ya kuonyesha kazi nzuri Brazili 2014, Waalgeria watakuwa na tumaini la kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2018 Urusi. Kufikia lengo hilo, wanatarajia kupata ushirikiano safi kutoka kwa wachezaji wao muhimu wanakipiga kwenye ligi kubwa za Ulaya, kama Yacine Brahimi, Sofiane Feghouli, Islam Slimani, Nabil Bentaleb na Carl Medjani ambaye ni nahodha wao.
Na moja ya mitihani yao ni kuifunga Tanzania ambayo imeshawatoa Malawi kwenye kinyang’anyiro.

 

Kocha

Vahid Halilhodzic hakuwa tayari kuongeza mkataba kuendelea kuinoa timu ya taifa ya Algerian tena, na aliondoka mara baada ya ziara yao ya Brazili kufika mwisho. Shirikisho la soka la Algeria likamteua kocha anayeaminiwa sana, Mfaransa Christian Gourcuff, ambaye majukumu yake ni kuiwezesha Algeria kushiriki Michuano ya Kombe la Afrika 2017 na Kombe la Dunia 2018 Urusi. Ni kocha mzoefu kwani amefundisha klabu za Ufaransa, na akifanikiwa atakuwa kocha wa kwanza mgeni kuiongoza Algeria Kombe la Dunia.

 

Takwimu

Algeria ni timu ya tatu ya Waarabu kufika raundi ya 16 Kombe la Dunia, baada ya Morocco kufika hatua hiyo pia kule Mexico 1986 na Saudi Arabia kule Marekani 1994.

Mfumo mwepesi kwa Taifa Stars

Taifa Stars: Ally Mustafa, Shomary Kapombe, Mwinyi Hajji, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Himid Mao, Thomas Ulimwengu, Said Ndemla, Mbwana Samatta, Mrisho Ngassa/Mudathir Yahya na Farid Mussa.

Kuifunga Algeria itakuwa ni mlima mkubwa na mgumu kwa Stars kupanda. Timu hiyo ya Waarabu ndicho kikosi bora zaidi katika mataifa ya Afrika kikiwa inashika nafasi ya 19 katika viwango vya FIFA kwahiyo ni dhahiri Tanzania inakwenda kukabili wababe wa soka Afrika.

Mfumo wa 4-4-2 umeonekana kuwa lugha nyepesi inayoelewaka kwa wachezaji wa Taifa Stars. Wanajua majukumu yao, wanayatimiza na kikubwa zaidi wanasahishana makosa yao uwanjani. Akikosea Cannavaro basi Yondani anasahisha makosa yake, akikosea Kapombe na kupitwa, Cannavaro hawi mbali kufuta makosa. Vivyo hivyo kwa Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu.

Akielezea kasoro chache za mfumo wa kikosi, Mbwana Samata amesema kuna wakati anashindwa kufunga mabao kutokana na aina ya mfumo wa uchezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars.

“Zipo kasoro kadhaa. Mfumo au aina ya wachezaji ambao ninashirikiana nao. Siwezi kusema wachezaji wa Tanzania ni wabovu, hapana ila nadhani mbinu na uzoefu mdogo wa mechi za kimataifa nalo ni tatizo,” alisema Samata.

Washambuliaji wengi wa Stars bado hawako makini, wanapoteza nafasi nyingi ambazo zote zilipaswa kuwa magoli, kwa mfano Samata alikosa goli la wazi ambalo kila mtu alishangaa ni kwanini alikosa Tanzania ilipocheza dhidi ya Malawi Dar es salaam dakika ya mwisho ya mchezo wa kwanza.

Uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga bado ni duni kwa kikosi cha Taifa Stars, safu ya kiungo haipo thabiti. Wakikutana na timu inayoshambulia kwa nguvu kama Algeria ni dhahiri watapoteana na watajikuta wakizuia hatari ya kufungwa kila mara.

Mara ya mwisho Stars kucheza dhidi ya Algeria walipata sare ya 1-1, hii inaashiria kuwa pamoja na uwezo mkubwa wa Algeria bado Stars wanaimudu na wakijidhatiti watashinda.

Jambo la muhimu ni kuhakikisha kikosi cha Mkwasa kinapata ushindi mnono nyumbani bila kuruhusu nyavu kuguswa.

No comments