HUU NI WAKATI SAHIHI WA POPPE KUJIVUA MAJUKUMU YAKE SIMBA SC, AMESHINDWA VIBAYA
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Wakati pambano la Yanga SC na
Toto Africans likiendelea katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baadhi
ya mashabiki wa klabu ya Simba SC walikuwa ‘wakisonokea’ utawala wa
klabu yao kwa kitendo cha kuwaacha wachezaji vijana ‘mazao ya klabu’ na
kuwasaini wachezaji wapya ambao si wa kiwango cha juu. Mfungaji namba
moja wa Toto ni kijana Miraj Athumani ambaye alitimiza goli lake la
tatu msimu huu katika kichapo cha 4-1 kutoka kwa Yanga siku ya jana
Jumatano.
Edward Christopher tayari
amefunga mago mawili msimu huu, wakati Abdallah Seseme, Hassan Khatib
wameendelea kucheza vizuri katika kiungo ( Seseme) na safu ya ulinzi (
Khatib). Vijana hao wanne walikuwa sehemu ya timu B ya Simba SC ambayo ‘
ilitingisha’ Tanzania Bara mwaka 2012.
Simba awali ilikuwa na mtazamo wa
kutumia wachezaji inaowazalisha yenyewe. Kwa maana ya kiushindani na
kibiashara lakini mtazamo huo umeshindikana kutokana na ‘propaganda’ za
viongozi wa juu wa klabu hiyo.
Leo hii Simba haipati huduma ya
Shomari Kapombe, Ramadhani Singano na badala yake vijana hao U23
wanaichezea Azam FC . Ni sababu za kimaslahi zilizowaondoa ndani ya
klabu hiyo. Nimewahi kuandika mara nyingi kuhusu mapungufu ya kiutendaji
ya mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.
Simba imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha pesa kuwasaini wachezaji wa
ndani na nje ya nchi bila kuzingatia aina ya wachezaji husika na
mahitaji ya timu kiujumla.
Sijawahi kuwa upande wa Poppe kwa
kuwa naamini kufanya hivyo ni sawa na kuendelea kushabikia hatua za
klabu kurudi nyuma badala ya kusonga mbele. Niseme wazi kuwa Singano
hakupaswa kuondoka Simba kwa sababu tu klabu ilishindwa kumpatia kiasi
cha pesa alichohitaji ili kusaini mkataba mpya.
Inasemekana kuwa mchezaji huyo
alihitaji kiasi cha milioni 50 lakini klabu iling’ang’ania kumsaini kwa
milioni 30 na baada ya mchezaji kukataa dau hilo yakatengenezwa
mazingira ya kumfunga kwa kigezo cha kuwa na mkataba nae, jambo ambalo
halikuwa na ukweli.
Mchezaji ambaye klabu imemlea kwa
miaka minne tena akiwa katika kiwango cha juu kama Singano hakupaswa
kuachana na Simba. Yeye pia hakupenda lakini aliamua kuchagua maisha
mengine Azam FC baada ya timu hiyo kumuheshimu. Kamati ya usajili ya
Simba imeshindwa kuwaheshimu wachezaji vijana ambao kwa hakika hivi sasa
ndiyo walistahili kulipa fadhila kwa kuwapa taji au nafasi ya pili
katika ligi kuu.
Klabu inakataa kumpatia Singano
milioni 50 lakini ina uwezo wa kusajili ‘wachezaji magarasa’ kutoka nje
ya nchi zaidi ya wawili. Hii yote ni kazi ya ‘Mr.Kazinyingi’ ambaye siku
zote anaamini katika matumizi ya hela ili kujenga timu.
Bahati mbaya kwa Poppe kila
wachezaji ambao wanaosajiliwa kwa gharama wanashindwa kuleta mabadiliko
katika timu. Na wale ambao wamekuwa wakiachwa na kujiunga na klabu
nyingine wamekuwa na mafanikio. Hii ni dalili ya kwamba Kamati hiyo ya
usajili ya klabu ya Simba haiwezi kuitengeneza timu mpya ya ushindi kwa
kuwa hawajui namna ya kutengeneza timu.
Jiulize tu, kwanini Kapombe,
Singano, Christopher, Miraj, Seseme, Khatib, Wiliam Lucian leo hii wapo
nje ya timu. Hawa ni vijana sita ambao walikuwa sehemu ya kikosi B
kilichoshinda mataji matatu mwaka 2012/13 katika michuano ya Super8,
Ujirani Mwema na Mapinduzi Cup baada ya utawala uliopita kuwapa nafasi
vijana hao huku timu A ikipambana kushinda ubingwa wa ligi kuu.
Sijawahi kuona ‘taswira’ ya Simba
kunyanyuka na kuleta ushindani katika ligi ikiwa chini ya Kamati ambayo
mara zote inawaza muda wa usajili ufike ili ipate nafasi ya kuwatema
wachezaji fulani na kuwasaini wachezaji wengine wapya hata kama hakuna
ulazima wa kufanya hivyo.
Ibrahim Twaha ni kijana ambaye
Simba ilimsaini kutoka Coastal Union akiwa na kiwango cha juu lakini
baada ya kuumia Kamati ya usajili ya klabu ilimtazama kama ‘mzigo’ hivyo
kama ilivyotoa kwa kundi la kina Miraji, Christopher, Singano, Khatib,
Lucian na Seseme hakupewa mkataba mpya lakini sasa anaendelea kuonesha
kiwango kizuri katika timu ‘dhaifu’ ya Coastal.
Vipi kuhusu kuachwa kwa Mrundi,
Amis Tambwe, kijana mwingine Haroun Chanongo msimu uliopita. Poppe
inawezekana hana ufahamu mkubwa kuhusu wachezaji anaokuwa akiwaacha ama
kuwasaini. Pia anajitambulisha kama kiongozi asiye na uwezo wa kuwasaini
wachezaji bora. Kwa hakika Kamati yake inaongoza kwa usajili wa
wachezaji wa hovyo zaidi klabuni hapo, pia ni Kamati ya usajili
iliyochemka zaidi kimaamuzi kwa kuwaacha wachezaji makini.
Simba itaendelea ‘kusafa’.
Itahangaika sana na kamwe nadiriki kusema utawala wa sasa unaweza
kumaliza miaka yao minne pasipo kushinda ubingwa wa ligi kuu kama tu
watashindwa kufikia maamuzi magumu ya kumuondoa Poppe katika nafasi
yake. Mara zote naamini kuwa ‘Mafanikio ndiyo kipimo sahihi cha ubora’
lakini bado sijayaona Simba tangu ikiwa chini ya Hans Poppe.
Tambwe, Elius Maguli,
Christopher, Chanongo, Singano, Seseme, Miaraj, Khatib, Lucian, Kapombe,
Twaha ni wachezaji 10 ambao hawakustahili kuachwa Simba SC. Pape Nd’aw,
Danny Sserunkuma, Paul Kiongera, Donald Musoti, Emily Namubona, Simon
Sserunkuma, Vicent Aghban, ni baadhi tu ya usajili usio na tija
uliofanywa na kamati ya usajili ya Simba SC.
Huu ni wakati sahihi wa Poppe
kujivua majukumu yake Simba na ajitolee kama mwanachama wa kawaida tu.
Nasikia sasa ‘Jicho kama ngumi kuelekea dirisha dogo la usajili’. Timu
gani kila baada ya kucheza gemu 5 inaomba muda wa usajili ufike….
No comments