RATIBA YA MECHI ZA LIGI YA VPL LEO NA DONDOO ZAKE
RATIBA HII HAPA
Ligi kuu Tanzania bara imeanza
kunoga, baada ya kumalizika kwa michezo ya mzunguko wa nne wikendi
iliyopita, Jumatano hii ligi hiyo inaendelea kwa michezo 7 kuchezwa
katika miji tofauti. Ni timu 3 tu ambazo hazijaangusha pointi hadi sasa.
Vinara Yanga SC wamekusanya alama
12 sawa na timu za Azam FC na Mtibwa Sugar, timu hizo zimeshinda gemu
zao zote nne zilizopita na kwanza msimu kwa 100% ya ushindi. African
Sport ya Tanga imefanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza msimu huu baada
ya kuishinda Ndanda FC goli 1-0 Jumapili na kuziacha Coastal Union na
JKT Ruvu katika kundi la timu ambazo bado hazijaonja ‘ladha’ ya ushindi
msimu huu.
Mgambo imekusanya alama
nne baada ya kufanikiwa kupata sare katika gemu moja na kushinda moja,
imeshindwa katika michezo mingine miwili sawa na Mbeya City na Ndanda
FC.
MTIBWA SUGAR v YANGA SC
Ni moja ya mechi kali katika
raundi ya tano msimu huu. Mechi hii itazikutanisha timu zenye uwiano
sawa wa pointi katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro Jumatano ya leo. Yanga
ina wastani wa magoli 10 ya kufunga na kufungwa kwa maana wamefunga
magoli 11 na kuruhusu nyavu zao mara moja.
Mtibwa ipo katika nafasi ya tatu
ikiwa na wastani wa magoli manne ya kufunga na kufungwa. Kikosi cha
kocha, Mecky Mexime kimefanikiwa kufunga jumla ya magoli 6 na kuruhusu
mawili katika gemu nne zilizopita. Huo utakuwa mchezo wa tatu mfululizo
kwa Mtibwa kucheza katika uwanja wa nyumbani wakati Yanga watakuwa nje
ya uwanja wa Taifa kwa mara ya kwanza msimu huu.
“Yanga ni timu nzuri ila
hawatishi, tutaendelea kuwafunga kila wanapokuja Morogoro” ni maneno ya
msemaji wa Mtibwa, Thobias Kifaru ambaye timu yake haijapoteza mchezo
dhidi ya Yanga tangu mwaka 2009 katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Yanga upande wao wamekuwa na ndoto ya kushinda gemu 10 mfululizo.
SIMBA SC vs STAND UNITED
Ni mechi nyingine kali ambayo
itapigwa leo katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Simba imepeleka
malalamiko yake kwa Shirikisho la soka nchini, TFF ikiwalalamikia
waamuzi waliochezesha pambano lao la Jumamosi iliyopita dhidi ya
mahasimu wao Yanga.
Katika mchezo huo, Simba
ilipoteza kwa kulazwa 2-0 na hivyo kuporomoka katika msimamo kutoka
nafasi ya pili hadi ya nne wakiwa na alama 9 baada ya kucheza gemu nne.
Wataikabili Stand United ambayo imeshinda michezo miwili mfululizo na
kuruka hadi katika nafasi ya sita wakiwa na alama 6.
Amri Kiemba, Nassoro Chollo,
Haroun Chanongo, Elius Maguli wataungana na kocha wao, Mfaransa, Patrick
Liewig kuikabili timu yao ya zamani. Simba haijawahi kuifunga Stand
katika michezo miwili waliyokutana katika ligi ya msimu uliopita.
Walilazimishwa sare ya 1-1 katika
uwanja wa Taifa na kuchapwa 1-0 katika uwanja wa Kambarage, Shinyanga
katika mchezo wa marejeano. Stand imefunga magoli matatu tu msimu huu
(yote yamefungwa na Maguli) na wameruhusu magoli matatu katika nyavu
zao.
Upande wa Simba, kiufungaji
hawajatofautiana sana na Stand kwani licha ya kufunga magoli 6 ni
wachezaji wawili tu waliofanikiwa kufunga magoli hayo, Mganda Hamis
Kiiza ambaye pia anashikilia kilele cha orodha ya wafungaji msimu huu
amefunga magoli matano na kiungo/mlinzi, Justice Majabvi amefunga goli
moja. Simba imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu.
AZAM FC v COASTAL UNION
Coastal wanasafa kupata ushindi
wa kwanza msimu huu. Wakiwa chini ya kocha, Mganda, Jackson Mayanja timu
hiyo ya Tanga ilipoteza michezo miwili ya ugenini na wakaambulia sare
mbili katika michezo miwili waliyocheza uwanja wao wa nyumbani,
Mkwakwani.
Coastal Union wanakutana na Azam
ambao wameshinda gemu zote nne zilizopita. Azam iliifunga Coastal 4-0
katika uwanja wa Azam Complex Chamanzi msimu wa 2013/14, wakashinda tena
2-0 msimu uliopita. Coastal haijafunga goli lolote msimu huu na
wameruhusu nyavu zao mara 3. Azam inashika nafasi ya pili ikiwa na alama
12 sawa na timu za Yanga na Mtibwa hadi sasa imefanikiwa kufunga juma
ya magoli 7 na kuruhusu mawili katika nyavu zao.
Azam inaweza kwenda kileleni mwa
msimamo wa ligi endapo itashinda mechi yao ya leo halafu Mtibwa na Yanga
zikatoka sare kwenye mchezo wao kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro
kwani endapo mtibwa na Yanga zikitoka sare zitakuwa na pointi 13 na
Azam kama watashinda leo watafikisha pointi 15.
Mambo si mazuri kwa kocha wa
Coastal Union, Jackson Mayanja kwani timu yake haina uwezo wa kufunga
magoli, anaweza kutimuliwa kama mambo yatazidi kwenda ‘mrama’.
AFRICAN SPORT v JKT MGAMBO
Tanzania Prisons iliichapa 1-0
Mbeya City FC katika mchezo wa kwanza wa ‘mahasimu wa mji’ msimu huu,
kisha Simba ikakubali kipigo cha 2-0 kutoka kwa Yanga, ‘Derby’ ya tatu
itapigwa leo Jumatano katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati kikosi
cha Sanifu Lazaro kitakapo wakabili maafande wa JKT Mgambo wanaonolewa
na Bakari Shime.
Sport imepata ushindi wa kwanza
msimu huu siku ya Jumapili baada ya kupoteza michezo mitatu mfululizo ya
kwanza. Ikiwa imeruhusu magoli matano na kufunga goli moja tu, Sport
wanaikabili Mgambo ambayo imepoteza michezo miwili, ikiwa imeshinda mara
moja na kupata sare katika gemu moja.
Mgambo ilichapwa 1-0 na Prisons
imefanikiwa kufunga magoli matatu na kuruhusu nyavu zao cheza mara nne,
ni timu yenye safu nzuri ya ulinzi lakini haina makali katika safu ya
mashambulizi kama ilivyo kwa wapinzani wao Sport.
TANZANIA PRISONS v MWADUI FC
Kikosi kilichotazamiwa kutamba
msimu huu ni cha Mwadui FC chini ya kocha, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’
kinaendelea ‘kusafa’ licha ya kukusanya wachezaji mastaa wenye uzoefu
kama, Shaaban Kado, Paul Nonga, Razaq Khalfan, Rashid Mandawa, Nizar
Khalfan, Said Sued, Malegesi Mwangwa, Jabir Aziz, Malika Ndeule, Bakari
Kigodeko, Anthony Matogolo, Athumani Idd ‘Chuji’ na wengineo.
Mwadui imeshinda mara moja tu
katika michezo minne iliyopita, imepoteza michezo miwili, sare imetoa
mara moja Jumamosi iliyopita walipolazimisha sare-tasa dhidi ya Coastal.
Prisons wameanza msimu kwa matokeo mazuri ya wastani, wameshinda gemu
mbili na kupoteza mbili. Mechi hii inazikutanisha timu zilizofunga
magoli mawili kila moja. Mwadui imeruhusu magoli mawili wakati Prisons
imeruhusu magoli matano
No comments